Jackson Numbi mmoja kati ya wagombea waliojitokeza kuwania nafasi hiyo jijini Mbeya.
Na Ripota Wetu, Mbeya
SIKU chache
baada ya CCM kumaliza zoezi la upigaji wa kura za maoni ndani ya chama hicho
jimbo la Mbeya mjini zimeibuka tuhuma kwamba mmoja wa wagombea Ubunge wa chama
hicho amewanunua viongozi wa chama wilaya kwa nia ya kutoa maoni ya kukubalika
kwake ndani na nje ya chama.
Taarifa za
ndani kutoka kwa baadhi ya wanachama hicho ambao hawakupenda kutajwa majina yao
walisema kuwa vikao vya chama vinaendelea ili kutoa upendeleo kwa mmoja wa
wagombea kwa madai ya kukubalika kwake ndani na nje ya chama.
Jumla ya
wagombea 16 wa CCM walijitokeza katika kuwania nafasi ya Ubunge wa jimbo hilo
ambapo walitembea katika kata 36 na kujinadi mbele ya wanachama na Agosti Mosi
wanachama walipiga kura na kuwapitisha wagombea wanaowahitaji.
Akizungumza
kwa njia ya simu juu ya kuwepo kwa madai hayo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Mbeya
Ephraim Mwaitenda ambaye kwa muda huo alidai yupo katika kikao alisema kuwa
kikao hicho kimeketi ili kutathmini wagombea wote walioshiriki katika
kinyang’anyiro hicho.
‘’Ni kweli
tupo kwenye kikao cha tathmini baada ya kura za maoni, tunaangalia kukubalika
kwa mgombea ndani na nje ya chama, hatupendi kurudia makosa ya mwaka 2010,
mwaka ule tulimpitisha mgombea Benson Mpesya aliyeongoza kwa kura lakini
matokeo yake tukashindwa vibaya kwenye uchaguzi mkuu,’’alisema.
Alisema
wanafanya tathmini ya kina kuangalia mgombea anayekubalika kwa vijana na kwenye
chama hatimaye watatoa maoni na mapendekezo yao na kuyapeleka kwenye vikao vya
juu vya chama.
‘’Kura
zilizopigwa hazitabadilishwa kila mgombea atabaki na kura zake kama
zilivyopigwa kwenye kura za maoni, hapa tunapitia uwezo wa mgombea mmoja mmoja
ndani ya chama na nje ya chama,’’alisema.
Hata hivyo
Mwaitenda baadaye alikata simu na kusema kuwa bado anaendelea na kikao na hivyo
atafutwe baadaye baada ya kumalizika kwa kikao.
Wagombea watatu
walioongoza katika kura hizo dhidi ya wenzao 16 ni Sambwee Shitambala(4,633),
Amani Kajuna(4,409),Charles Mwakipesile(2,316).
|