Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) juzi aligeuka mbogo na kutaa kupokea
taarifa ya maendeleo iliyotolewana na Kaimu MKurugenzi wa Halmashauri ya wilaya
ya Chunya, Mbeya, Charles Mwakalila, baada ya kubainika kufichwa kwa mambo
muhimu hususani takwimu sahihi za Fedha za miradi elimu, barabara na Maji.
Waziri Ghasia aligomea taarifa hiyo juzi mbele ya
watumishi wa idara mbalimbali wa halmashauri hiyo wakati wa kikao baina yake na
watumishi aliowakutanisha kwa lengo la kuwasikiliza kero zao na kuzijibia.
Aidha, Waziri Ghasia, alianza kubaini madudu
hayo mwanzoni kabisa mwa ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo
ukiwemo wa mradi wa ujenzi wa chumba cha Maabara kwa Shule ya Sekondari ya
Chokaa ambapo alionesha wasiwasi wake baada Kaimu Mkurugenzi, Mhandisi wa
majengo wilaya Mkombozi Cyrille na Ofisa mipango wilaya, Erasto Mbilinyi,
kutaja viwango vya fedha vinavyotofautiana ya ujenzi wa chumba hicho.
“Jamani siwezi kuweka jiwe la msingi kwenye mradi huu
wenye ubabaishaji kwani nauliza benki ya dunia imelewatea kiasi gani Mkurugenzi
anasema Sh270 milioni, mhandisi anasema 176 haya Ofisa mipango hapa naye ana
jibu lake na hamjui kama mimi najua fika fedha zilizoletwa hapa halafu
mnanidanganya,” alisema Waziri.
Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro
alimuomba radhi kwa mkanganyiko huo na kumsihi kuweka jiwe hilo jambo
ambalo Waziri alifungua jiwe hilo kwa shingo upande tena kwa kutumia mkono
mmoja wa kushoto huku akitazama pembeni badala ta kusoma maandishi yaliyokuwa
yameandikwa kwenye jiwe hilo.
Hata hivyo hali ikawa tete zaidi ndani ya kikao na
watumishi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali
ambapo alisema kuwa hawezi kupokea taarifa iliyojaa taarifa za kizushi huku
akibainisha wazi mambo ya msingi ambayo yanatakiwa yawekwe wazi kwa wananchi
yamefichwa
“Hapa haiwezekani hawa wakuu wa idara lazima kuna kitu
mheshimiwa Mkuu wa Mkoa kwanini wanaficha takwimu sahihi na muhimu za fedha za
umma na kila mkuu wa idara nikimuuliza fedha za mradi fulani ziko wapi
anashindwa kuzisemea na Mkurugenzi wenyewe anaongopa hata kiasi cha fedha
alizosaini mbele yangu za miradi ya maji, nasema hivi hii taarifa
sipokei,”alisisitiza Waziri Ghasia.
Alisema kuwa katika ziara yake alitegemea kupewa
taarifa za miradi iliyotengewa bajeti kwa kuzingatia vipaumbele vilivyopo kwenye Mpango wa
matokeo makubwa sasa (BRN) lakini imekuwa kinyume chake huku kukiwa na majibu
sahihi juu ya fedha hizo zimekwenda wapi.
Aidha, Waziri alisema kuwa miongoni mwa miradi
ambayo fedha yake wakurugenzi walishasainishwa ni pamoja na fedha za miradi ya
maji, barabara na elimu lakini matokeo yake hakuna hata kimoja kati ya hivyo
vinavyooneshwa kama utekelezaji wake umefikia wapi.
Baada ya mkanganyiko huo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro aliposimama alisema kuwa hata yeye anashindwa kuelewa mdudu
aliyewachanganya watumishi hadi hadi kufikia kujikanyaga kanyaga ovyo ovyo
mbele yake.
Na
Godfrey Kahango,Chunya
0 comments:
Post a Comment