Pages

Sunday, January 26, 2014

KANDORO AIKATAA TAARIFA YA MATUMIZI YA FEDHA ZA MIRADI


Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro akiwa katika moja ya mikutano yake katika ziara ya siku tatu Wilaya ya Mbozi Mkoani  Mbeya



Mkuu wa Mkoa wa Mbeya   Abbas Kandoro aikataa taarifa ya matumizi ya fedha zaidi ya Sh 174 milioni za  miradi miwili ya  bwawa la maji katika kijiji cha Iyula na Msia Wilayani Mbozi  na kutoa wiki moja kwa halmashauri ya Wilaya kutoa maelezo ya sahihi ya miradi hiyo.

Katika  fedha hizo,  Sh 134 milioni zimetumika katika mradi wa  bwawa la maji  katika kijiji cha Iyula huku fedha zilizopokelewa  kutoka serikalini zikiwa Sh 250 milioni  na nyingine ni  Sh40milioni za mradi wa bwawa la maji la kijiji cha Msia ambapo fedha hizo zimetumika huku mradi ukiwa bado haujaaanza kutekelezwa.


Akizungumza wakati alipotembelea miradi hiyo Kandoro alisema kuwa katika mradi wa bwawa la Iyula taarifa ya mkaguzi inaonyesha kuwa  fedha zilizopokelewa  ni Sh250milioni na zilizotumika  ni Sh134milioni ”fedha zingine zimekwenda wapi kwani akaunti ya kijiji zilitolewa fedha zote  Sh250milioni na mbaya zadi mmeomba fedha zingine  nahitaji maelezo sikubaliani na taarifa yenu ”alisema 

Kuhusu mradi wa bwawa la Msia Kandoro alisema kuwa  hakubaliani taarifa ya mtumizi ya fedha hizo ambazo ni Sh40milioni kwani hakuna kazi iliyofanyika zaidi ya michoro,utafiti na semina.

“Siwezi kukubali  kiurahisi  hii taarifa yenu kwani fedha zilizotumika ni nyingi sana lakini maelezo ya matumizi haya  haziendani  ni lazima timu ya waataalam wangu watafika hapa kufanya uchunguzi wa kina  ili kubaini  fedha  zilizotumika zinaendana na kazi iliyofanyika”alisema

Alisema kuwa serikali Mkoa  haiwezi kukubali kuona fedha za miradi  ya maendeleo ya wananchi zinatumika vibaya na kwamba yeyote atakaye bainika kuhusika na ubadhilifu wa fedha hizo ikiwa ni pamoja na kubadilisha matumizi iliyokusudiwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.

“Na hili nasema halikubaliki lazima hatua kali zitachukuliwa na ikibidi watu watapelekwa polisi na yeyote atakayebainika kuhusika na ubadhilifu huu atakamatwa na polisi kwani fedha nyingi za serikali zinaletwa huku lakini hazitumiki kama ilivyokusudiwa”alisema 

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya mradi wa bwawa la maji la Iyula Jua Mwamlima alisema kuwa  walipokea fedha  katika akaunti ya kijiji  Sh250 milioni na fedha hizo zilitolewa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza zilitolewa Sh115milioni na awamu ya pili zilitolewa Sh134milioni.

“Lakini kwenye taarifa inaonyesha fedha zilizotumika katika mradi huu ni Sh134milioni hivyo hata sisi kama uongozi wa kamati hatujui hayo mahesabu yamekaaje kwani kwenye akaunti ya kijiji fedha zote zilishatolewa”alisema 

Naye  Mwenyekiti wa kamati ya mradi wa bwawa la Msia Godwell alisema kuwa fedha hizo walizitumia kwa ajili ya semina kwa viongozi wa kijiji ,kuwalipa watu waliofanya utafiti na wataalam wa mkichoro kwa ushauri wa ofisa  kutoka ofisi ya halmashauri ya Wilaya.

0 comments: