Pages

Monday, December 9, 2013

Busokelo washauliwa kufanya shughuli za ufugaji nyuki

Mkuu wa Wilaya ya Rungwe Crispin Meela

Imeelezwa kuwa  Wakazi wa Halmashauri ya Busokole Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya wanaweza kuondokana na umasikini  endapo kama watashiriki katika  kutunza misitu kwa  kufanya shughuli za  ufugaji  wa nyuki na kupata  Asali na Nta.

Akizungumza  na Wenyeviti  kutoka vijiji  56  Mtendaji Kuu wa  shirika la  Elimisha , Festo Sikagonamo alisema kuwa wenyeviti hao wanapaswa  kufanya utambuzi wa misitu katika maeneo ya vijiji vyote  na kuyatunza  na kuhifadhi ili iweze kuwasaidia katika kuondokana na umasikini.



Alisema  kuwa    elimu  inahitajika  kwa wananchi juu ya uhifadhi  na  kwamba   wanawajibu wa kujadili kwa pamoja namna  ya kuanzisha miradi mbadala endelevu ambayo ni  rafiki na mazingira ikiwa ni pamoja na miradi  ya kufuga nyuki kwa lengo la kujipatia Asali na Nta

“Kwa sasa soko la  Asali lipo wazi kwani ni bidhaa mbayo inahitajika sana kwa matumizi mbali mbali ya binadamu hivyo  mnapaswa kutumia  nafasi mlionayo kwa kuwaelimisha wananchi mnaowaongoza kuacha kufanya uhalibifu wa misiti na badala yake  kutunza misitu hiyo kwa kufanya shughuli za ufugaji wa nyuki”alisema

Naye  Mkuu wa  Wilaya Rungwe Crispin Meela amewataka wenyeviti hao wa vijiji  kuondoa woga wakati wa kusimamia uharibifu wa misitu  iliyopo katika vijiji husika.

“Utunzaji wa misitu upo mikononi mwenu  hivyo hakikisheni mnafanya  kazi hiyo bila kumwogopa mtu yeyote yule,hawa wenzetu wanasiasa  najua ni ngumu sana kulisemea hili kwani wengi wanaogopo kuwaonya wananchi kwa kuogopa kunyimwa kura”alisema Mkuu huyo wa wilaya.

 Kwa upande wao Wenyeviti hao  walisema  kuwa wazee wa mila wamekuwa hawana mwamko wa kutunza  misitu kutokana na  jamii kuwadharau  wazee hao na hivyo kuacha misitu kuendelea kuteketea pasipo uangalizi.

“Wazee wa mila wakithaminiwa  na vijana wanaoishi vijijini suala la utunzaji  Misitu litakuwa endelevu na hakuna mtu ambaye atajihusisha na uharibifu wa misitu hasa ya asili.”alisema  Mwenyekiti  wakijiji cha Kandete Jobu Mwasipilege

Alisema kuwa kutokana na uharibifu wa misitu uliopo hivi sasa ipo haja kwa serikali kuanza kutoa elimu kwa wazee wa mila  ili kuendelea kutunza misitu hiyo ambayo hivi sasa imeharibiwa  vibaya na vijana kutokana na shughuli za kijamii.

“Unajua ndugu zangu wenyeviti zamani mzee wa mila alikuwa akisema jambo  lilikuwa linaeleweka  kwani kutokana na nguvu za kuaminika katika jamii  kuwa mzee wa mila ni kila kitu hivyo hakuna mtu ambaye alikuwa akithubutu kujaribu kukata misitu au kufanya uharibifu wowote kutokana na kuambiwa kuwa katika misitu hiyo kuna  nyoka mkubwa ambaye anadhulu watu hivyo  kutokana na kauli hizo hakuna kijana aliyekuwa akijaribu kufika katika misitu hiyo”alisema Mwenyekiti huyo.

Naye Mwenyekiti wa  Kijiji cha Mwela Aman Kyambinga alisema kuwa kufuatia uharibifu huo wa misitu serikali za vijiji bado zinatakiwa  kuwaita wazee wa mila na kuwa karibu nao kutokana na  kauli za wazee hao wa mila kwa jamii kuwa na ushawishi  kwa wananchi  na kukubalika .


0 comments: