Pages

Monday, December 2, 2013

Madiwani chadema kushitakiwa

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Athanas Kapunga (wa kwanza kushoto) akifafanua jambo kwa waandishi wa habari wakati akielezea hatua watakazochukua dhidi ya baadhi ya madiwani wa Chadema wanaodaiwa kughushi saini za madiwani wenzao.




Baraza la madiwani katika halmashauri ya jiji la mbeya  jana limeazimia kuwachukulia hatua za kisheria  baadhi ya Madiwani  waChadema  kwa tuhuma za kugushi  saini za madiwani  kwa lengo la kudai  kuitishwa  kwa mkutano  maalum   wa  kujadili kutofuatwa kwa ratiba vikao vya  halmashauri na kuhitaji ufafanuzi kuhusu matumizi shilingi milioni 100 kwa safari ya Mkurugenzi na Meya wa jiji nchini  China.

Aidha baraza hilo pia limeazimia kuwashitaki katika kamati ya  maadili  baadhi ya madiwani  ambao walitoa lugha za matusi katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi baada ya kukataliwa kujadiliwa kwa hoja hizo katika baraza hilo kutokana na taarifa ya maombi  iliyowasilishwa kutokidhi vigezo.


Madiwani   wa kambi ya upinzani  waliwasilisha taarifa ya hoja  waliyotaka ijadiliwe katika   kikao  hicho cha baraza   iliyohusu    kuhitaji  ufafanuzi  wa safari ya china iliyohusisha Mstaki Meya,Mkurugenzi  mtendaji  wa halmashauri,Mchumi na Mwenyekiti wa kamati ya mipango na uchumi kwa madai kuwa haikuwa na tija na masilahi ya Wananchi wa jiji la Mbeya  na barua ya kuomba kuitishwa kwa  mkutano maalum.

Akizungungumza na Waandishi wa habari Mstahiki Meya wa jiji la Mbeya  Atanas  Kapunga alisema kuwa  halmashauri  ilipokea  barua kutoka kwa madiwani 19,  Novemba 07,mwaka huu  wakiomba kuitishwa kwa mkutano maalum ambapo   alidai saini    za madiwani watano kati ya hayo ziligushiwa.

“Baada ya kupitia majina na saini zao ilibainika kwamba takribani majina matano saini zake hazikuwa zinalingana na zile zilizoonekana katika daftari la mahudhurio ambalo hutumika wakati wa vikao vya halmashauri na mengine kuonekana kuandikwa na mtu mmoja  kilichoashiria kuwepo kwa  dalili za kughushi”alisema 

Alisema kuwa  pia katika orodha hiyo ya majina yalikuwepo baadhi ya majina ambayo madiwani wake hawakuwepo kutokana na sababu mbali mbali “kwa mfano Diwani wa kata ya,  Foresti Boyd Mwabulanga yupo  jijini Dar es salaam kwa zaidi ya mwezi mmoja  kwenye matibabu na Mbunge Joseph Mbilinyi alikuwa akihudhulia bunge  lakini jina lake liliorodheshwa na kuwekwa saini ambayo siyo yake”alisema 

“ Kutokana na kubaini kuwepo kwa tatizo hilo kikao cha baraza la madiwani  na wao wakiwepo kwani walijiorodhesha kwenye   daftari ya mahudhurio na kusaini posho kimeazimia hatua za kisheria zichukuliwe  na kwa wale waliotoa lugha za matusi kushitakiwa kwenye kamati ya maadili ya halmashauri ya jiji la Mbeya.”alisema.

Akizungungumzia safari ya nchini China, alisema safari hiyo iligharimu shilingi milioni 57 na kwamba ulikuwa ni mualiko kutoka Ofisi ya waziri Mkuu na kwamba safari hiyo ilishirikisha pia waurugenzi na Mameya kutoka majiji mengine nchini. 

Akizungumzia  tuhuma hizo Diwani  wa kata ya Mwakibete (CHADEMA ), Lucas Mwampiki  alisema kuwa uwamuzi huo ni dalili za kujihami na kwamba hakuna saini iliyokuwa imegushiwa “kama wanadhani sisi tumegushi saini je wamewauliza hao wenye majina kama saini zao zimegushiwa mimi nafikiri suala hili tuachie vyombo vya kisheria vichunguze kwa umakini na ndipo vitueleze kama tumeghushi na CCM kuhusu kutoa lugha za matusi wao  madiwani wa ndiyo walianza kutoa lugha hizo na hata kufikia kutupiga kwani kuna madiwani wawili wa Chadema  walipigwa”alisema 

 Aidha alisema kuwa suala hilo wameliwasilisha kwenye chama na kwamba chama ndicho kitaamua nini kifanyike kutokana na yale waliyofanyiwa katika mkutano huo ambao wanadhani ni kinyume cha sheria na kanuni za mikutano ya mabaraza ya madiwani.










0 comments: