Pages

Thursday, August 28, 2014

WAFANYAKAZI WA TAZARA WATISHIA MGOMO BARIDI KWA KUTOLIPWA MIEZI MITANO

 WAFANYAKAZI TAZARA WATISHIA MGOMO BARIDI KWA KUTOLIPWA MIEZI MITANO
Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi SUGU akipewa maelezo na mmoja wa wafanyakazi wa Reli ya TAZARA ambao hawajalipwa mishahara kwa miezi mitano.


 
Baadhi ya wafanyabiashara wa Reli ya TAZARA wakimsikiliza Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi alipowatembelea kusikiliza matatizo yao.

Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi akizungumza na wafanyakazi wa TAZARA baada ya kupata maelezo juu ya tatizo lao la kukosa mshahara kwa miezi mitano


Mmoja wa wafanyakazi wa TAZARA ambaye ni dereva wa Treni Chrisant Amani akisisitiza jambo juu ya tatizo lao la kukosa mshahara kwa miezi mitano.

Mfanyakazi wa TAZARA akisisitiza jambo juu ya kukosa mshahara kwa miezi mitano

 
 
Wafanyakazi wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA) upande wa Tanzania kituo cha Mbeya wameitisha mgomo baridi kwa kutofanya kazi wala kuendesha mitambo hadi pale watakapolipwa mishahara yao ya miezi mitano wanayolidai Shirika hilo.
Wafanyakazi hao takribani 40  ambao wanadai kuwawakilisha wenzao zaidi ya 1000 wanaofanyakazi katika Reli hiyo kati ya Tunduma na Kurasini walitoa msimamo huo mbele ya Mbunge wa Jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi huku wakimuomba kukifikisha kilio chao Wizara ya Uchukuzi.
‘’Tunakuomba Mheshimiwa Mbunge, tufikishie kilio chetu  Wizarani, tuko hoi tunakufa na njaa, tunadaiwa kodi za nyumba ,karo za shule watoto wamefukuzwa, maisha yanazidi kuwa magumu siku hadi siku,’’alisema Ramadhani Mohamed aliyejitaja kuwa ni Karani Mwandamizi wa Shirika hilo.
Naye Chrisant Amani aliyejitaja kuwa ni Dereva wa Treni alisema kuwa mazingira magumu waliyonayo yamewasababisha kushindwa kuendesha Treni na kuwa hawezi kuendesha Treni katika mazingira aina hiyo hadi hapo atakapohakikishiwa amelipwa mishahara yake anayolidai Shirika.
‘’Mimi ni Dereva wa Treni, siwezi kuendesha treni nikiwa na mawazo na mazingira magumu huku nikiwa nimebeba roho za watu,ninaweza kusinzia kwa njaa nikapoteza mwelekeo, ni hatari kufanya kazi katika hali hii,’’alisema Amani.
Kwa upande wake Hilda Mtaya ambaye anafanya kazi ya Kufungua Njia, ‘Point Man’ alisema kuwa watoto wake wamefukuzwa shule na nyumba aliyopanga kafukuzwa anaishi kwa rafiki yake hivyo anahitaji kulipwa mshahara wake ili atatue matatizo yake vinginevyo ataendelea na mgomo hadi atakapothibitishiwa malipo yake.
Mtaya alisema kuwa Shirika hilo ni la Tanzania na Zambia lakini wafanyakazi na kuwa hali ya kipato kati ya wafanyakazi wa pande hizi hailingani kwa kuwa wenzao wa Zambia wana maisha mazuri kuliko wao wa upande wa Tanzania.
Akizungumza juu ya sakata hilo Mbunge wa Mbeya mjini, Mbilinyi alisema kuwa amesikia kilio chao na kuahidi kulifikisha suala hilo Wizarani na kuenda mbali zaidi kwa kubainisha kuwa watendaji wa wizara hiyo akiwemo Waziri anayehusika hawana nia ya dhati kutafutia ufumbuzi  tatizo hilo.
''Huu ni ubabaishaji, wafanyakazi wanafikisha hadi miezi mitano Wizara haishituki, wamekaa maofisini hawajui matatizo ya wafanyakazi wao, hii inasikitisha,''alisema.
Mbilinyi alisisitiza kuwa matatizo mengi yaliyopo katika Reli ya TAZARA yanatokana na watendaji kuwa na maslahi binafsi hali ambayo inaleta hisia kuwa wapo baadhi ya viongozi(hakufafanua ni viongozi gani)  ni wamiliki wa magari makubwa yanayosafirisha mizigo nje ya nchi hivyo kufilisika kwa Shirika hilo kuna maslahi kwao.
Alisema kuwa amekuwa akipigia kelele suala la uboreshaji wa reli hiyo kwa  muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuimarishwa kwa Bandari ya Nchi Kavu iliyopo Iyunga jijini Mbeya ambayo anaamini ingesaidia kupunguza kero na kuboresha utendaji wa Shirika hilo lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea.

Gazeti hili liliwasiliana kwa njia ya simu na Meneja mkuu wa TAZARA upande wa Tanzania Abdallah Shekimweri ili kuzungumzia tatizo la wafanyakazi hao na kusema kuwa mtoa taarifa wa Shirika hilo ni Ofisa Uhusiano aliyemtaja kwa jina la Regina Tarimo ambaye alipotafutwa alidai kuwa analifanyia kazi jambo hilo na atapiga simu kwa mwandishi wa habari hizi baadaye ili kutoa ufafanuzi wa suala hilo. 
Kwa hisani ya www.mkwinda.blogspot.com

0 comments: