MTOTO Vivian Philipo(12) akichota maji kwenye mfereji kutokana na uhaba wa maji katika kijiji cha Izumbwe Wilaya ya Mbeya vijijini .
WANANCHI wa kata ya Igale Wilaya ya Mbeya vijijini
wamelalamikia ucheweleshwaji wa kukabidhiwa
mradi wa maji na kusababisha usumbufu kwa wakina mama na watoto kutembea
umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta maji.
Wakizungumza na
Mwananchi kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa vijiji vya Izumbwe na Itaga walisema kuwa
katika maeneo yao hakuna maji ya bomba kutokana na mradi huo kutokabidhiwa na
hivyo wananchi kushindwa kuvuta maji.
“Kuna mradi wa maji katika kata yetu ya Igale na tumesikia
kuwa mkandarasi amechelewa kuukabidhi mradi huu kwa madai kuwa bado hajalipwa fedha na halmashauri hali ambayo inaleta usumbufu mkubwa
na kusababisha kutumia maji ya mito na mifereji”alisema Joyce Mwakalinga mkazi
wa kijiji cha Izumbwe
Mwakalinga alisema kutokana na mradi huo kutoanza kufanya kazi,umeleta usumbufu mkubwa kwa wanafunzi ambapo
wamekuwa wanapoteza muda mwingi wa masomo na kwenda kutafuta maji kwa ajili ya
matumizi ya nyumbani.
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Igale,Alinanuswe
Mwakamala alisema kuwa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 80 na kwamba bado
serikali haijatoa fedha kwa mkandarasi ili aweze kukamilisha sehemu iliyobakia
na kuukabidhi.
Alisema kuwa gharama ya ujenzi wa mradi huo ni Sh1.2bilioni
na kwamba una miaka miwili tangu ulipoanza ujenzi wake na kwamba upaswa kukamilika
ndani miezi sita na mwaka mmoja wa nusu ulikuwa ni kwa ajili ya matazamio.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Upendo Sanga alisema kuwa tatizo la
kutokamilika na kukabidhiwa kwa mradi huo wa maji ilikuwa ni ukosefu wa fedha
lakini kwa sasa tayari mkandarasi ameshalipwa fedha wiki iliyopita hivyo
atakamilisha kazi yake na kukabidhi mradi huo.
Na Brandy Nelson
0 comments:
Post a Comment