WAJAWAZITO. wa kata ya Igale wilayani
Mbeya mkoani hapa wamelalamikia kufukuzwa na kunyimwa huduma za uzazi kutoka
kwa baadhi ya watoa huduma katika zahanati za vijiji kwa madai ya kuwa wananuka.
Hayo yameelezwa juzi wakati wa
mrejesho wa yaliyojiri kwenye utafiti wa siku tano uliofanywa na maofisa wa
Mtandao wa Jinsia wa TGNP kwenye kata ya Igale wilayani Mbeya juu ya tatizo la
huduma za kijamii zinazotolewa kwa wakazi wa vijiji vitano vya Horongo, Izumbwe,
Shongo na Igale.
Akizungumza katika kikao
kilichowahusisha wanahabari wa vyombo mbalimbali mkoani Mbeya, Naye Mwenyekiti
wa Kituo cha Taarifa na Maarifa TGNP kata ya Igale Lyidia Sankemwa alisema kuwa
akina mama wajawazito wamekuwa wakifukuzwa kwenye zahanati wakidaiwa kuwa ni
wachafu wananuka.
‘’Tumepokea malalamiko mengi kutoka
kwa wakina mama wajawazito kuwa baadhi
ya watoa huduma za afya katika zahanati
zetu huwafukuza akina mama wajawazito, kwa madai kuwa
wananuka na hatinaye kucheweleshewa kupatiwa huduma,’’alisema
Alifafanua kuwa tatizo hilo limekuwa
kubwa maeneo ya vijijini kutokana na kukosekana huduma za uzazi kwa akina mama
na mtoto na kuwa katika baadhi ya maeneo akina mama husafiri zaidi ya kilomita
10 kufuata huduma ya wazazi.
Naye katibu wa kituo hicho, Alfred Mwambugu alisema kuwa
kutokana na tatizo hilo baadhi ya akina
mama wamekuwa wakikata tamaa ya kwenda kupata huduma katika zahanati hizo kwa
kuhofia kutolewa lugha chafu na hivyo
kujifungulia nyumbani hali ambayo ni hatari kwa maisha yao.
Akizungumzia malalamiko hayo Ofisa
habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Hamza Mwangomale alisema ameyapokea malalamiko hayo na kwamba tayari ameshawasiliana na mratibu wa afya kwa
ajili ya kwenda kufanya kikao cha pamoja na watoa huduma za afya katika
zahanati hizo.
“Hili suala ninauwezo nalo
nitalishughulikia mara moja ili kuhakikisha malalamiko hayo yanafanyiwa kazi
tunaandaa utaratibu wa kukutana na watoa huduma za afya katika kata hiyo ya
igale ili kuweza kulizungumza kwa pamoja
na kuchukua hatua kwa wale watakaobainika wanatabia hizo”alisema
Kwa upande wake Ofisa Mtendaji wa
Kata ya Igale Alinanuswe Mwakamala , alisema
kata hiyo yenye jumla ya vijiji vitano ina zahanati nne ambazo
hazitoshelezi kwa kuhudumia wakazi wote wa kata hiyo hali ambayo inasababisha
baadhi ya akina mama kuchelewa kupatiwa huduma hiyo kwa wakati.
Alisema kata hiyo ina jumla ya wakazi 11,800 ambao
hupata huduma kwenye zahanati nne na kuwa kijiji kimoja cha Horongo hakina
zahanati hivyo wakazi wake hulazimika kufuata huduma hiyo kwenye zahanati za
vijiji vingine umbali wa kilomita tano.
0 comments:
Post a Comment