OFISA Mtendaji na
Mwenyekiti wa kitongoji cha Nsalala Wilaya
ya Mbeya mkoani hapa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuuza ardhi
ya kijiji kwa Sh8.6 milioni bila ridhaa
ya wananchi
Tukio hilo lilitokea katika
mkutano wa hadhara uliofanyika juzi baada ya wananchi kuwatuhumu viongozi hao
kwa kuuza mali ya umma kisha kuziweka fedha hizo kwenye akaunti zao binafsi.
Wakizungumza katika mkutano huo
wananchi hao walisema baada ya kubaini wizi huo walimwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Wilaya ya Mbeya Upendo Sanga wakitaka
kuundwa kwa Tume ya uchunguzi ili kubaini fedha zinazodaiwa kuhodhiwa na
viongozi hao bila ridhaa ya wananchi.
Baada ya kupokea malalamiko
hayo Mkurugenzi aliituma tume ya uchunguzi ambapo ilibaini tuhuma mbalimbali
dhidi ya viongozi hao na kusoma maagizo mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika
juzi katika uwanja wa shule ya msingi
Nsalala.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya wananchi Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya
Prosper Msivala, alisema uchunguzi umebaini kuwa Mwenyekiti anatuhumiwa kwa makosa kushiriki kuuza mali ya
Umma kinyume cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011.
Makosa mengine yanayomuhusisha mwenyekiti huyo ni pamoja na
kutuhumiwa Kutunza fedha zilizotokana na mauzo hayo kwenye akaunti zake binafsi
mbili zilizopo Benki ya NMB Mbalizi Road zenya namba 6251000804 na 62510009.
Kwa upande wa mtendaji wa
kitongoji hicho mwanasheria huyo alisema
kuwa anatuhumiwa kwa kuwa na matumizi
mabaya ya madaraka kwa kushindwa kusimamia Kitongoji na kuwapotosha
wananchi,kughushi nyaraka na mihutasari ya vikao nakukodisha eneo la maziko kwa
shughuli za kilimo bila kufuata taratibu.
“Mtendaji pia anatuhumiwa kuuza
mali ya umma kinyume na taratibu ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011,matumizi mabaya
ya muhuri ambao siyo halali,kumdanganya Mwajiri kwa kuficha ardhi ya Mamlaka na
kutokabidhi kwa mamlaka”alisema
Mwanasheria huyo aliongeza kuwa
kutokana na makosa hayo Mkurugennzi Mtendaji wa Wilaya ameagiza eneo lililouzwa
kurudishwa mara moja kwenye Mamlaka ya Mji mdogo kanzia sasa.
Maagizo mengine ni pamoja na Mtendaji wa Kitongoji kusimamishwa kazi
kuanzia mara moja ili kupisha uchunguzi
wa tuhuma zinazomkabili na kuagiza vyombo vya Dola kumchukulia hatua kali za
kisheria Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nsalala.
Baada ya Mwanasheria kumaliza kuisoma barua hiyo kutoka kwa
Mkurugenzi viongozi hao wote kwa pamoja walichukuliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano
maalum.
Diwani wa Kata ya
Nsalala Kissman Ngomale alifunga mkutano kwa kuwataka wananchi kuwa wavumilivu
ili kusubiri sheria ichukue mkondo wake dhidi ya viongozi hao ikiwa ni pamoja na
kufikishwa mahakamani.
Brandy Nelson
0 comments:
Post a Comment