WAJUMBE
wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wamesema Mgodi wa makaa ya mawe Kiwira umejaa
figisufigisu na ulikabidhiwa kwenye Shirika la Madini la Taifa (Stamico) ukiwa kama maiti isiyo na mwenyewe.
Wabunge hao
walitoa kauli hiyo juzi walipofika eneo la mgodi ambapo wengine walimtaja Rais
wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kuwa ameongeza ugumu wa kuwapata wawekezaji
wapya katika mgodi huo.
Walitoa
maoni hayo baada ya kupokea taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) Zena
Kongoi ambaye alisema alikabidhiwa mgodi
huo Juni 30, 2014 ili auendeshe na kuusimamia kufuatia hatua za Serikali
kutengua uamuzi wake wa 2005 kuubinafsisha kwa mwekezaji Tan Power Resources
(TPR).
Kongoi
alisema malengo ya mradi ni kuzalisha umeme wa megawati 200 , lakini gharama za
uwekezaji zinazohitajika ili kuanza kazi hiyo ni dola 468 milioni za Marekani
na kwamba yapo makaa ya kutosha kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 11.
Mbali ya
gharama hizo pia wafanyakazi 893 wanadai zaidi ya Sh1 bilioni na kwamba Shirika
lake liliomba fedha mara kadhaa za kuanza kazi za awali na kuwalipa wafanyakazi hao lakini bado hawajapata na kwamba upo
uwezekano gharama za kufufua mgodi zikazidi kupanda.
“Kwa sasa
Shirika linaendelea na mchakato wa kumpata mwekezaji, lakini bado hatujampata
kutokana na sababu mbalimbali.”alisema
Mbunge wa
Bukoba Mjini , Wilfred Lwakatare akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo
alisema Stamico ni kama waliuziwa gari bila kupewa kadi yake.
‘’ Stamico
ni kama mmekabidhiwa maiti isiyo na ndugu je Tan Power Resources ni ile ya Yona na Mkapa? Kama ndiyo basi mjue kazi ipo. Ndiyo maana Serikali haitoi
fedha , hapo ni figisufigisu tu’’, alisema.
Naye Suzan
Kiwanga (Mlimba) alishangaa kuona Wachina waliujenga mgodi huo na kuwaachia
Stamico waliouendesha kwa miaka 17 na baadaye kuuza kwa bei ya kutupa ambaye
alidai aliuendesha mgodi huo kwa miaka mitatu na hatimaye kuacha ‘kaburi ambalo
alisema sasa wabunge wanataka lifukuliwe ili kujua nani alizikwa’’,
Naye
Mbunge wa Nkasi Ally Keissy alipasua jipu akisema wawekezaji walioondoka kwenye mgodi huo
waliutumia mgodi kupata fedha za mkopo kwenye benki na mfuko wa hifadhi za
jamii (majina yanahifadhiwa).
“Mwekezaji
alipewa mgodi kwa Sh7 bilioni, lakini alilipa Sh2 bilioni mpaka sasa hajalipa na sasa benki zinadai,
wafanyakazi wanadai, je kweli mgodi utapata mwekezaji mwingine? alihoji
Mbunge wa
Msalala, Ezekiel Maige alishauri kabla
ya kuwatafuta wawekezaji wengine, Stamico itoe taarifa sahihi za tathimini je
mwekezaji atapata faida akitumia zaidi ya dola milioni 470 za Marekani
kuwekeza, Je mgogoro wa wafanyakazi ana madai ya wafanyakazi unaisha lini, je
leseni ya mgodi ipo kwa nani na mwekezaji
aliyeondoka kwa nini asihusike katika kutatua kero za wafanyakazi.
Ndipo Makamu
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ussi Salim Pondeza alipomtaka Kaimu Mkurugenzi ajibu
maswali yote kwa maandishi akiwa na vielelezo vyote tangu mgodi huo
ulipoanzishwa.
Pondeza alisema
kamati yake pia itataka majibu jinsi Serikali ilivyompatia mwekezaji na
alivyofanya na hatimaye kuuacha mgodi huo
na kwamba taarifa zote ziwe na vielelezo sahihi.
Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa James Mdoe alipoulizwa kama anaweza
kujibu maswali alisema atasimamia majibu yote yapatikane kwa muda ulipopangwa.
Story kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment