Pages

Sunday, January 26, 2014

Wakulima Mbozi walia na soko huria



Wakulima  katika kata ya Harungu Wilaya ya Mbozi Mkoani Mbeya  wamesema kuwa kuwepo kwa soko   huria kumechangia   mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani kutotekelezwa na kusababisha maghala kutotumika kwa muda mrefu na kuua vyama vya ushirika. 


Akizungumza kwa niaba ya Wakulima hao  mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro mara baada ya kutembelea kata hiyo  mjumbe wa bodi  ya chama cha msingi cha ushirika  kata ya Harungu  Andrew Nyingi  alisema kuwa   Wakulima wamekuwa wakiuza mazao yao yakiwa bado shambani kwa bei ndogo .

Alisema kuwa kwa upande wa zao la kahawa wachuuzi wamekuwa wakiwashinikiza wakulima kununua kahawa mbichi ikiwa bado shambani  huku maghala yaliyojengwa kwa malengo ya kutumia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani yakikaa bila kutumika  kwa muda mrefu.

“Haya maghala kwa sasa ni mabovu na hayajatumika kwa muda mrefu  na  kutokana na kuwepo kwa soko huria na mazao yetu kukosa soko la uhakika kwani wanunuzi wamekuwa wakinunua mazao yetu shambani bila kuwepo kwa utaratibu “alisema

Naye  Kaimu Mkurugenzi  wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi  Dk. Charles 
Mkombacheka  alisema kuwa  kuna jumla ya maghala 54 yaliyojengwa   kwa nguvu za Wananchi miaka ya 80 katika Wilaya hiyo lakini  hayatumiki,  na kwamba kati  ya hayo  28 yanatarajiwa kuanza kufanyiwa ukarabati  ambao unakadiliwa kugharimu Sh 1.4 bilioni .

Kwa upande Mkuu wa Mkoa wa Mbeya  Abbas Kandoro  alisema kuwa  ni lazima ushirika urudishwe  na kuimalisha  vikundi vidogo vya wakulima  na kuyafufua maghala hayo  kwa   kuendeleza mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ili kumsaidia mkulima kupata soko la uhakika wa mazao yao na kuondokana na umasikini.

Aidha kandoro alisema kuwa  ni lazima wakulima kuwa na  uelewa wa mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani  hivyo Serikali inawajibu wa kuhakikisha elimu hiyo inatolewa ili kuweza  kumsaidia mkulima katika shughuli nzima ya kilimo  chenye manufaa.

“Mfumo huu stakabadhi  ya mazao  maghalani unamlinda mkulima hivyo hatunabudi  kuhakikisha wakulima wanapatiwa elimu kwanza na ndipo tuanze kuutekeleza mfumo huu  na kurudisha vyama vya ushirika ambavyo ndiyo msimamizi  wa mkulima katika upatikanaji wa soko la uhakika la mazao yao”alisema

0 comments: