Pages

Tuesday, April 5, 2016

Mgodi wa makaa ya Mawe Kiwira umejaaa Figisufigisu


WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,  wamesema Mgodi wa makaa ya mawe Kiwira umejaa figisufigisu na ulikabidhiwa kwenye Shirika la Madini la Taifa (Stamico)  ukiwa kama maiti isiyo na mwenyewe.
Wabunge hao walitoa kauli hiyo juzi walipofika eneo la mgodi ambapo wengine walimtaja Rais wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kuwa ameongeza ugumu wa kuwapata wawekezaji wapya katika mgodi huo.
Walitoa maoni hayo baada ya kupokea taarifa ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji  wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) Zena Kongoi  ambaye alisema alikabidhiwa mgodi huo Juni 30, 2014 ili auendeshe na kuusimamia kufuatia hatua za Serikali kutengua uamuzi wake wa 2005 kuubinafsisha kwa mwekezaji Tan Power Resources (TPR).
Kongoi alisema malengo ya mradi ni kuzalisha umeme wa megawati 200 , lakini gharama za uwekezaji zinazohitajika ili kuanza kazi hiyo ni  dola 468 milioni  za Marekani  na kwamba yapo makaa ya kutosha kuzalisha umeme kwa zaidi ya miaka 11.
Mbali ya gharama hizo pia wafanyakazi 893 wanadai zaidi ya Sh1 bilioni na kwamba Shirika lake liliomba fedha mara kadhaa za kuanza kazi za awali  na kuwalipa wafanyakazi  hao lakini bado hawajapata na kwamba upo uwezekano gharama za kufufua mgodi zikazidi kupanda.
“Kwa sasa Shirika linaendelea na mchakato wa kumpata mwekezaji, lakini bado hatujampata kutokana na sababu mbalimbali.”alisema
Mbunge wa Bukoba Mjini , Wilfred Lwakatare akizungumza baada ya kupokea taarifa hiyo alisema Stamico ni kama waliuziwa gari bila kupewa kadi yake.
‘’ Stamico ni kama mmekabidhiwa maiti isiyo na ndugu je Tan Power Resources  ni ile ya Yona na Mkapa? Kama ndiyo basi  mjue kazi ipo. Ndiyo maana Serikali haitoi fedha , hapo ni figisufigisu tu’’, alisema.
Naye Suzan Kiwanga (Mlimba) alishangaa kuona Wachina waliujenga mgodi huo na kuwaachia Stamico waliouendesha kwa miaka 17 na baadaye kuuza kwa bei ya kutupa ambaye alidai aliuendesha mgodi huo kwa miaka mitatu na hatimaye kuacha ‘kaburi ambalo alisema sasa wabunge wanataka lifukuliwe ili kujua nani alizikwa’’,
Naye Mbunge  wa Nkasi  Ally Keissy alipasua jipu akisema  wawekezaji walioondoka kwenye mgodi huo waliutumia mgodi kupata fedha za mkopo kwenye benki na mfuko wa hifadhi za jamii (majina yanahifadhiwa).
“Mwekezaji alipewa mgodi kwa Sh7 bilioni, lakini alilipa Sh2 bilioni  mpaka sasa hajalipa na sasa benki zinadai, wafanyakazi wanadai, je kweli mgodi utapata mwekezaji mwingine? alihoji
Mbunge wa Msalala, Ezekiel Maige  alishauri kabla ya kuwatafuta wawekezaji wengine, Stamico itoe taarifa sahihi za tathimini je mwekezaji atapata faida akitumia zaidi ya dola milioni 470 za Marekani kuwekeza, Je mgogoro wa wafanyakazi ana madai ya wafanyakazi unaisha lini, je leseni ya mgodi ipo kwa nani na  mwekezaji aliyeondoka kwa nini asihusike katika kutatua kero za wafanyakazi.
Ndipo Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Ussi Salim Pondeza alipomtaka Kaimu Mkurugenzi ajibu maswali yote kwa maandishi akiwa na vielelezo vyote tangu mgodi huo ulipoanzishwa.

Pondeza alisema kamati yake pia itataka majibu jinsi Serikali ilivyompatia mwekezaji na alivyofanya na hatimaye kuuacha mgodi huo  na kwamba taarifa zote ziwe na vielelezo sahihi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa James Mdoe alipoulizwa kama anaweza kujibu maswali alisema atasimamia majibu yote yapatikane kwa muda ulipopangwa.

Story kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

0 comments: