Pages

Sunday, April 3, 2016

Mtendaji,Mwenyekiti Kitongoji cha Nsalala washikiliwa kwa tuhuma za ubadhilifu

OFISA mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha nsalala wakipandishwa kwenye gari ya polisi mara baada ya kusomwa kwa taarifa ya tume ya uchunguzi na kutuhumiwa kuhusika na uuzaji wa ardhi ya kijiji kwa Sh8.6 milioni na fedha hizo kuziweka kwenye akaunti zao binafsi.


MWANASHERIA wa halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Prosper Msivala akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi mtendaji inayohusu tuhuma za ubadhilifu dhidi ya ofsa nmtendaji na mwenyekiti wa kitongoji Nsalala

WANANCHI wa kitongoji cha Nsalala Wilaya ya Mbeya wakisikiliza taarifa inayowahusu Ofisa mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha Nsalala kutuhumiwa kuuza ardhi ya kijiji kwa Sh8.6milioni bila ya ridhaa ya wananchi 






OFISA  Mtendaji na Mwenyekiti wa kitongoji cha Nsalala  Wilaya ya Mbeya mkoani hapa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuuza ardhi ya kijiji  kwa Sh8.6 milioni bila ridhaa ya wananchi
Tukio hilo lilitokea katika mkutano wa hadhara uliofanyika juzi baada ya wananchi kuwatuhumu viongozi hao kwa kuuza mali ya umma kisha kuziweka fedha hizo kwenye akaunti zao binafsi.
Wakizungumza katika mkutano huo wananchi hao walisema baada ya kubaini wizi huo  walimwandikia barua Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Upendo  Sanga wakitaka kuundwa kwa Tume ya uchunguzi ili kubaini fedha zinazodaiwa kuhodhiwa na viongozi hao bila ridhaa ya wananchi.
Baada ya kupokea malalamiko hayo Mkurugenzi aliituma tume ya uchunguzi ambapo ilibaini tuhuma mbalimbali dhidi ya viongozi hao na kusoma maagizo mbele ya mkutano wa hadhara uliofanyika juzi  katika uwanja wa shule ya msingi Nsalala.
Akisoma taarifa hiyo  mbele ya wananchi  Mwanasheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya Prosper Msivala, alisema uchunguzi umebaini kuwa Mwenyekiti  anatuhumiwa kwa makosa kushiriki kuuza mali ya Umma kinyume cha sheria ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011.
Makosa mengine  yanayomuhusisha mwenyekiti huyo ni pamoja na kutuhumiwa Kutunza fedha zilizotokana na mauzo hayo kwenye akaunti zake binafsi mbili zilizopo Benki ya NMB Mbalizi Road zenya namba 6251000804 na 62510009.
Kwa upande wa mtendaji wa kitongoji hicho  mwanasheria huyo alisema kuwa anatuhumiwa  kwa kuwa na matumizi mabaya ya madaraka kwa kushindwa kusimamia Kitongoji na kuwapotosha wananchi,kughushi nyaraka na mihutasari ya vikao nakukodisha eneo la maziko kwa shughuli za kilimo bila kufuata taratibu.
“Mtendaji pia anatuhumiwa kuuza mali ya umma kinyume na taratibu ya manunuzi ya Umma ya mwaka 2011,matumizi mabaya ya muhuri ambao siyo halali,kumdanganya Mwajiri kwa kuficha ardhi ya Mamlaka na kutokabidhi kwa mamlaka”alisema
Mwanasheria huyo aliongeza kuwa kutokana na makosa hayo Mkurugennzi Mtendaji wa Wilaya ameagiza eneo lililouzwa kurudishwa mara moja kwenye Mamlaka ya Mji mdogo kanzia sasa.
Maagizo mengine ni pamoja na  Mtendaji wa Kitongoji kusimamishwa kazi kuanzia mara moja  ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili na kuagiza  vyombo vya Dola kumchukulia hatua kali za kisheria Mwenyekiti wa Kitongoji cha Nsalala.
Baada ya Mwanasheria kumaliza kuisoma barua hiyo kutoka kwa Mkurugenzi viongozi hao wote kwa pamoja  walichukuliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano  maalum.
 Diwani wa Kata ya Nsalala Kissman Ngomale alifunga mkutano kwa kuwataka wananchi kuwa wavumilivu ili kusubiri  sheria ichukue mkondo wake  dhidi ya viongozi hao ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.
Brandy Nelson









0 comments: