Pages

Thursday, January 9, 2014

Kanisa la moravian jimbo la kusini Magharibi laingia katika mgogoro mkubwa




 KANISA la  Moravian jimbo la Kusini Magharibi  limeingia katika mgogoro mkubwa  baada ya bodi ya kanisa hilo  kumsimamisha  kazi  Mwenyekiti  wake  Mchungaji Nosigwe Buya  na kudaiwa kubadilisha vitasa vya mlango wa ofisi yake huku  mwenyekiti huyo akikaidi kusimamishwa kwake na  kuahidi kuendelea kutoa  huduma kwa waumini .

Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi Mwenyekiti  huyo Mchungaji  Nosigwe Buya kuhusu kusimamishwa kwake alisema kuwa hakubaliani na hatua hiyo kwani barua aliyokabidhiwa ya kusimamishwa kwake  haikujitosheleza kutokana na kutoonyesha sababu za kusimamishwa.


“Ni kweli nimekabidhiwa barua  ya kusimamishwa  kwangu  ya tarehe Januari 03,2014  ambayo imeeleza kuwa nimesimamishwa kazi ya Uwenyekiti hadi mwaka 2016 katika mkutano wa sinodi ya  uchaguzi  kwa makosa 11 na Bodi ya Kanisa itanipangia  kituo kingine cha  kazi” 

“ Kutokana na barua hiyo sijatendewa haki kwani hadi sasa sijui makosa yangu  kwani awali  nilikubali kusimamishwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai,31 hadi Oktoba kwa lengo la kuipisha tume kufanya uchunguzi juu ya matumizi ya fedha Sh200 milioni za  mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya Mbozi “alisema 

Alisema kuwa baada ya bodi kumsimamisha katika kipindi hicho cha miezi mitatu aliongozewa miezi mingine  miwili  na ndipo ilipofika  Januari 03,2014 alikabidhiwa  barua ya kusimamishwa hadi mwaka 2016 wakati wa sinodi ya uchaguzi.

 Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa  makanisa ya Moravian Afrika alisema kuwa hadi sasa uongozi wa kanisa hilo haujatoa ripoti ya tume kwa waumini na wachungaji na kwake  na  badala yake  umechukua uwamuzi wa kumsimamisha  bila kuelezwa sababu 11 zilizotajwa katika barua hiyo.


“Msimamo wangu kwa sasa mimi bado ni Mwenyekiti na nitaendelea kuhudumia waumini wangu pamoja na kuwa tayari ofisi yangu wamebadilisha kitasa na kuu funga na nimeandika barua ya kuitisha  mkutano wa Sinodi ya dharula ambapo wajumbe wake ni Wachungaji na mjumbe mmoja mkristo kutoka kwenye ushirika   ambayo itafanyika  January 18,2014  katika kanisa la Bethrehem eneo la mama John”alisema 

Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa  makanisa ya Moravian Afrika alisema kuwa lengo la kuhitisha Sinodi hiyo ni kuwataka waumini na Wachungaji kupata ukweli  na kama kuna makosa”nipo tayari kujihudhuru  na kuacha nafasi yangu ichukuliwe na mtu mwingine”alisema

Wakizungumzia mgogoro huo baadhi ya wachungaji ambao hawakutaka majina yao kutajwa gazetini walisema kuwa kilichofanyika katika jimbo hilo ni kutaka kuleta mpasuko ndani ya kanisa kwani hata barua walizokabidhiwa kuhusu kusimamishwa kwa Mwenyekiti hazijaeleza sababu ya kusimamishwa kwake.

“Kama wachungaji tunasikitishwa na hatua ya jambo hili ilipofikia na kwa sasa tunashuhudia wazi kuwepo kwa mpasuko mkubwa ndani ya kanisa kwani nasi hatutakubaliana  ni hii hali kama mwenyekiti amebainika kuwa na makosa ni vema tukajulishwa ili tuweze kufahamu kama kuna halali kusimamishwa au kaonewa kama anavyodai yeye”alisema  mmoja wa Wachungaji hao

Katibu  Mkuu wa jimbo  hilo Willey Mwasile  alipohojiwa kuhusiana na tukio hilo alikiri kuwepo na kwamba kwa sasa msemaji wa jimbo hilo ni Makamu Mwenyekiti Mchungaji  Zakaria Sichone “hivyo nakushauri ukamuone ndiye anaweza kutoa maelezo hayo yote “alisema 

Kwa upande wake Makamu mweyekiti wa jimbo hilo  Mchungaji  Zakaria Sichone alipotakiwa kueleza sababu za kumsimamisha Mwenyekiti huyo alisema  kuwa hilo jambo  linahusu   mambo ya kiroho  na kumtaka mwandishi  kusubiri hadi hapo kikao cha   halmashauri  kuu kinachotarajjia kufanyika siku ya ijumaa kwa ajili ya suala hilo.

“Ni kweli  waumini wanahaki ya kufahamu ukweli kuhusuana na jambo hili  lakini pia Mwenyekiti amekiuka taratibu kwa kuamua kuingia ofisini na kuendelea na kazi wakati tayari alikuwa ameshasimamishwa  tangia awali na yeye kukabidhi ofisi hivyo   nakuomba  ndugu mwandishi  nitakutafuta kwa ajili ya kukueleza hili suala mara baada ya bodi  na halmashauri kuu kukutana”alisema

0 comments: