Pages

Monday, March 28, 2016



MTOTO Vivian Philipo(12)  akichota maji kwenye mfereji  kutokana na uhaba wa maji katika kijiji cha Izumbwe Wilaya ya Mbeya vijijini .




WANANCHI  wa kata ya Igale Wilaya ya Mbeya vijijini wamelalamikia ucheweleshwaji wa kukabidhiwa  mradi wa maji na kusababisha usumbufu kwa wakina mama na watoto kutembea umbali mrefu  kwa ajili ya kutafuta maji.

Wakizungumza  na Mwananchi kwa nyakati  tofauti  baadhi ya wananchi wa  vijiji vya Izumbwe na Itaga walisema kuwa katika maeneo yao hakuna maji ya bomba kutokana na mradi huo kutokabidhiwa na hivyo wananchi kushindwa kuvuta maji.

“Kuna mradi wa maji katika kata yetu ya Igale na tumesikia kuwa mkandarasi amechelewa kuukabidhi mradi huu kwa madai  kuwa bado hajalipwa fedha  na halmashauri hali ambayo inaleta usumbufu mkubwa na kusababisha kutumia maji ya mito na mifereji”alisema Joyce Mwakalinga mkazi wa kijiji cha Izumbwe

Mwakalinga alisema   kutokana na mradi huo kutoanza kufanya  kazi,umeleta usumbufu mkubwa kwa  wanafunzi   ambapo wamekuwa wanapoteza muda mwingi wa masomo na kwenda kutafuta maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya Igale,Alinanuswe Mwakamala alisema kuwa ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 80 na kwamba bado serikali haijatoa fedha kwa mkandarasi ili aweze kukamilisha sehemu iliyobakia na kuukabidhi.

Alisema kuwa gharama ya ujenzi wa mradi huo ni Sh1.2bilioni na kwamba una miaka miwili tangu ulipoanza ujenzi wake na kwamba upaswa kukamilika ndani miezi sita na mwaka mmoja wa nusu ulikuwa ni kwa ajili ya matazamio.

Mkurugenzi Mtendaji wa  Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya,Upendo Sanga alisema kuwa tatizo la kutokamilika na kukabidhiwa kwa mradi huo wa maji ilikuwa ni ukosefu wa fedha lakini kwa sasa tayari mkandarasi ameshalipwa fedha wiki iliyopita hivyo atakamilisha kazi yake na kukabidhi mradi huo.

Na Brandy Nelson

0 comments: